WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikijipanga wakuchukulia hatua wabunge wake waliosaliti msimamo wa Kamati Kuu na kuhudhuria vikao vya Bunge la Katiba, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda ametangaza kutogombea ubunge tena kupita chama hicho.
Shibuda, Said Arfi (Mpanda Mjini) na Leticia Nyerere (Viti Maalum) wamewasili mjini Dodoma na kujisajili kwa lengo la kushiriki vikao hivyo, licha ya kuzuiliwa na chama chao ambacho kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kimesusia Bunge hilo.
Shibuda alitangaza uamuzi huo kwa nyakati tofauti jana, wakati akizungumza na wazee wa mji wa Maswa na Malampaka wilayani humo, walipotaka kujua hatima yake ya kisiasa ndani ya CHADEMA.
Alidai kauli za vitisho na kejeli dhidi yake zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA, ndizo zimemfanya achukue hatua hiyo.
“Mimi niliingia CHADEMA kwa hiari yangu baada ya kuona dhuluma zilizokuwa ndani ya CCM, chama ambacho kimenilea kisiasa, nikaona heri niende CHADEMA ambako nilidhani kuna demokrasia na ukombozi wa kweli.
“Lakini nilichokikuta humo ni tofauti, kwani kila siku wazee wangu mnasikia napata misukosuko isiyo na maana,” alisema.
Shibuda alisema pamoja na mambo yote hayo, amekuwa kimya muda mrefu hata ilifikia wakati vijana ndani ya chama wakimtukana matusi huku wakitumia maneno mbalimbali ya kumdhalilisha kwa kumwita msaliti na pandikizi la CCM.
“Pamoja na shutuma zote zinazotolewa juu yangu na kupachikwa majina mbalimbali, hata siku moja sijawahi kuitwa katika Kamati Kuu ya CHADEMA na kuhojiwa,” alisema.
Akizungumzia tuhuma zilizotolewa juu yake kuwa alikiuka katazo la kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea, alisema hazina msingi wowote, kwani hajahudhuria kikao hicho wala hakuchukua posho.
Shibuda alikiri ni kweli alifika mjini Dodoma akitokea Dar es Salaam akiwa njiani kuelekea jimboni kwake, na alipita bungeni kwa ajili kufuatilia fedha za matibabu kutokana na kusumbuliwa na mguu.
“Nasumbuliwa na mguu na siye tunatibiwa na serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kipindi chote unapokuwa mbunge, sasa kosa langu la kuitwa msaliti hapa ni lipi na hata hiyo posho wanayodai nimeichukua iko wapi,”alisema.
Alisisitiza kuwa tangu habari hizo zianze kuandikwa na kutangazwa katika vyombo vya habari, hajawahi kuulizwa na kiongozi yeyote wa CHADEMA isipokuwa amesikitishwa na kauli ya Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu ya kutishia kumfukuza kwa usaliti.
Akizungumzia UKAWA, alisema kuwa yeye si sehemu ya kundi hilo na wala hajawahi kuelimishwa juu ya kundi hilo, bali anachokumbuka kuwa kupitia viongozi wa juu wa vyama vya upinzani vya CHADEMA, CUF na NCCR walikubaliana katika kikao kuwa wabunge wao wasishiriki vikao hivyo hadi hapo rasimu iliyoletwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba itapoheshimiwa.
“Mwislamu hawezi kutetea Uislamu kama hajui nguzo saba za Uislamu na pia huwezi kuwa Sheikh bila kupitia Madrasa na hata katika Ukristo huwezi kuutetea Ukristo kama hujui Biblia na hukusoma mafundisho na mie siwezi kuwa UKAWA wakati sijaelimishwa juu ya kundi hilo,” alisema.
Alipoulizwa na Wazee ni chama kipi ambacho atagombea katika uchaguzi mkuu ujao, alisema wakati ukifika atasema, kwani kwa sasa bado anatimiza wajibu wake wa kuwatetea wapiga kura wake.
Chanzo; Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment