TANZANIA YAGUNDUA GESI ASILIA YENYE UJAZO WA TRILIONI 50.5
Na Anitha Jonas – Maelezo.
Tanzania imegundua gesi asilia katika maeneo 19 ya
mwambao na kina kirefu cha maji baharini ambayo ina
ujazo wa trilioni 50.5.
Kati ya maeneo hayo 19 yaligundulika gesi hiyo ,matano
yanapatikana katika mwambao na 14 yapo katika kina
kirefu cha maji baharini .
Hata hivyo gesi iliyogundulika katika maeneo ya mwambao
kama Songo songo na Mnazi Bay kwa sasa inatumika
kufua umeme na pia kwa ajili ya matumizi ya viwandani,
majumbani na kwenye magari.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas
Kandoro wakati akifungua kongamano la wadau wa mafuta
na gesi linalofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo
Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa huyo amewataka wadau hao watumie
muda wao kutoa maoni yatakayosaidia kuwa Sera
ya Mafuta na Gesi asilia itakayowanufaisha watanzania
pindi itakapoanza kutumika.
Kandoro ameongeza kuwa ni vema Sera hiyo ikasaidia
Serikali kupata mapato yake yatakayotokana na Mafuta
na Gesi asilia kwa ajili ya kuleata maendeleo
mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wake.
“Uandaaji wa sera hii ulipitia marejeo ya nyaraka mbalimbali
ikiwemo sera ya petroli za nchi zilizogundua nishati ya
mafuta na gesi asilia zikiwemo Uganda,Ghana,Sierra Leone
na Pakistani”.
Mpaka Oktoba mwaka jana (2013) Serikali ilikuwa imekamilisha
sera ya gesi asilia ,hii ni kwa ajili ya kutoa muongozo wa
kusimamia na kuendesha biashara ya gesi asilia katika
uchakataji,usafirishaji na usambazaji”, alisema Kandoro.
Amesema kuwa Sera hiyo itazingatia na kuangalia kwa
ukaribu suala la udhibiti wa mazingira ukomo wa uzalishaji
wa rasilimali hiyo pale utakapoanza.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Jiolojia kutoka
Wizara ya Nishati na Madini Adam Zuberi amesema lengo
a sera hiyo ni kuhakikisha rasilimali ya gesi asilia
inawanufaisha watanzania wote kwa mapato
yatakayopatikana katika maeneo husika kwani asilimia
3 itabaki Halmashauri kwa matumizi ya wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Prof. Ibrahim Lipumba ameishauri Serikali kuwa
makini katika makubaliano na makampuni yatakayochimba
gesi katika mgawanyo wa mapato kama inavyoonyesha
katika sera kuwa asilimia 60 ya mapato itapelekwa Serikalini.
Pia umakini na uangalifu wa hali ya juu unahitajika kwenye
makubaliano hayo.
Mkutano huo wa wa siku moja uliandaliwa na wizara ya Nishati
na Madini na kujumuisha wataalam mbalimbali waliobobea
katika masuala ya mafuta ,wawakilishi wa ofisi za ubalozi
zilizopo nchini ,Vyama vya siasa , viongozi wa dini, Wakuu wa
Mikoa na asasi za kiraia .
No comments:
Post a Comment